Mwandishi wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, Martin Fletcher akiwa katika chumba cha kuhifadhi meno ya tembo katika Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam ambako zaidi ya meno 34,000 yamehifadhiwa. Picha ya Daily Mail.
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Mwandishi huyo anaripoti kuwa; “Wahisani ambao wangeweza kutoa fedha hizo, walikejeli kiwango hicho wakisema hakina uhalisia.”
Dar es Salaam. Licha ya Rais Jakaya Kikwete kutoa ahadi ya kuteketeza maelfu ya meno ya tembo yaliyo kwenye ghala la Serikali, imeelezwa kuwa uwezekano huo ni mdogo.
Mwandishi wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, Martin Fletcher ameeleza kushtushwa na hali ya ulinzi kwenye ghala hilo lililosheheni meno 34,000 ya tembo ambayo kwa biashara ya magendo nchini China yanagharimu Pauni 150 milioni za Kiingereza (Sh403.5 bilioni)
Fletcher, ambaye aliandika habari ya kuhusika kwa wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa wa Tanzania katika biashara haramu ya meno hayo kiasi cha kuifanya nchi kuwa muuzaji mkuu wa nyara hizo, aliandika hayo kwenye taarifa kuhusu ziara yake nchini iliyochapishwa na gazeti hilo jana.
Habari ya awali ilitikisa ulimwengu ambao unapambana kulinda viumbe walio hatarini kutoweka ikiwatuhumu wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa nchini kuhusika, huku Serikali ikishindwa kuwadhibiti.
Habari hiyo iliifanya Serikali ya Tanzania kufungua milango kwa vyombo vya habari vya nje kuja nchini kupata habari sahihi kuhusu tatizo hilo, akiwamo Fletcher wa Daily Mail.
Katika ziara yake, Fletcher alipata nafasi ya kutembelea ghala la nyara hizo, kuzungumza na maofisa wanyama pori pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
“Nyalandu pia aliweka bayana kuwa uteketezaji wa shehena ya Tanzania ni kitu ambacho kiko mbali na uhalisia, licha ya ahadi ya Kikwete jijini London,” Fletcher alimkariri Nyalandu kwenye habari hiyo ambayo imeambatana na picha alizozielezea kuwa za kushtua za ghala hilo, lenye idadi kubwa ya meno ya tembo kuliko maghala yote duniani.
“Alisema Rais alikuwa na nia ya kuteketeza (shehena hiyo), lakini Tanzania ilitaka ilipwe takriban Pauni 30 milioni za Uingereza kutoka Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya Mfuko wa Hifadhi ya Tembo.”
Hata hivyo mwandishi huyo anaripoti kuwa; “Wahisani ambao wangeweza kutoa fedha hizo, walikejeli kiwango hicho wakisema hakina uhalisia.”
Alipoulizwa kuhusu kauli hiyo jana, Nyalandu alisema baadhi ya mambo kwenye habari ya mwandishi huyo yamekuzwa, lakini alisema uamuzi wa kuteketeza nyara hizo haujafikiwa.
Alisema Serikali ilichofanya hadi sasa ni kupiga marufuku biashara zote za meno ya tembo, hivyo haitauza yaliyopo na haitaomba kibali tena cha kufanya biashara hiyo na kwamba kinachoendelea sasa ni mazungumzo ya namna ya kushughulika na shehena iliyopo.
“Meno mengine yaliyopo ni ya kihistoria. Ni marefu kuliko mengine na tembo wa aina hii hawapo tena, hivyo kuwa nayo pia ni kitu kizuri. Haya meno ni mali ya Watanzania wote, uamuzi wa kuyateketeza lazima uchukuliwe kwa busara,” alisema.
Kwa mujibu wa Fletcher meno mengine yana urefu wa futi 7, uzito wa tani 125 na moja linaweza kubebwa na watu kuanzia watatu, huku jino fupi likiwa na uzito wa kilo 0.4500 na kwa mujibu wa jangili aliyekiri kuua tembo 30 kwa siku, jino hilo dogo liling’olewa kutoka kwa tembo mtoto.
Mara tatu katika kipindi cha miaka minane, Tanzania imeomba bila mafanikio kibali cha kuuza shehena yake kutoka katika nchi 180 zilizosaini makubaliano ya kudhibiti biashara ya kimataifa ya viumbe walio hatarini kutoweka, Cites, licha ya ushahidi mkubwa kuwa kitendo cha kuuza mara moja tu, kitazidisha tamaa ya China kupata meno hayo.
Akizungumzia ziara yake nchini, mwandishi huyo anaelezea udhaifu katika ulinzi wa ghala hilo lililo nyuma ya jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam.
“Ghala hilo niligundua siyo kama ngome (yenye ulinzi mkali). Lina milango ya chuma ya kusukuma ikiwa na kufuli nzito tano ambazo funguo zake zimegawanywa kwa maboharia wawili, lakini milango ilifunguliwa yote nilipofika,” makala hiyo inaeleza. “Kila jino limewekwa alama na namba na ghala ina kamera za ulinzi wa ndani, lakini sikuona mlinzi mwenye silaha nje.”
Mwandishi huyo anaeleza kuwa habari yake ya kwanza iliyohoji kama mtoto wa Mfalme wa Wales na Waziri Mkuu wanaweza kushikana mkono na Rais Kikwete wakati alipotembelea Uingereza, ilizua kizaazaaa kiasi cha Rais Kikwete kuitisha kikao na maofisa waandamizi wa Maliasili na kutoa maelekezo kuwa wafanye kazi.
Mwandishi huyo alitembelea maghala ya meno ya tembo, Hifadhi ya Selous ambayo mwaka 2006 ilikuwa na tembo 70,000 lakini hadi sasa wamesalia 13,000 tu. Baadhi ya meno yalichukuliwa kutoka tembo waliokufa na mengi kukamatwa kutoka kwa majangili na hayawezi kuuzwa kwa sababu ya biashara hiyo kuzuiwa duniani.
0 comments: