Ikiwa ni takribani mwezi mmoja tu tangu bomu lilipolipuka kwenye mkutano
wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoani Arusha, jana
tukio kama hilo lilitokea jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa Mbunge
wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, ambao aliutishia kwa lengo la
kuwaelezea wananchi mrejesho wa yaliyojiri bungeni hivi karibuni na
kuhamasisha wananchi kushiriki kutoa maoni kwenye rasimu ya Katiba mpya.
Tofauti na Arusha, jana bomu hilo lililipuka likiwa kwenye gari la
Polisi waliokuwa kwenye mkutano huo katika viwanja vya Sahara, katika
Kata ya Mabibo jijini Dar es Salaam na kuibua taharuki kubwa kwa
wananchi na wafuasi wa Chadema waliokuwa wamehudhuria mkutano huo.
Polisi wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba bomu hilo lililipuka kwa bahati mbaya na kwamba ni la jeshi hilo.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa
Wilaya ya Kinondoni, Yusuf Mrefu, alisema mlipuko huo ulitokea kwa
bahati mbaya na kwamba haikuwa nia ya polisi kutumia nguvu au kuzuia
mkutano wa Chadema.
"Ni bomu la mkononi. Polisi walikuwa na mazungumzo na viongozi wa
Chadema na siyo kwamba kulikuwa na vurugu au matumizi ya nguvu, ni tukio
la bahati mbaya," alisema.
Mrefu alisema pia kwamba Polisi haikuwa imepanga kupiga mabomu kwenye mkutano huo wala kuuzuia.
"Siwezi kueleza limetengenezwa wapi, ni aina gani au kazi yake; kwa
sababu mimi mwenyewe nimepewa taarifa kwa simu, sikuwa eneo la tukio,
nilikuwa kwenye msafara wa Makamu wa Rais," alisema.
Aidha, Kaimu Kamanda huyo bila kufafanua alisema: "Halina madhara." Hata
hivyo, alipoulizwa kazi ya bomu hilo ikiwa halina madhara, alijibu
kwamba asingeweza kueleza zaidi kwa kuwa hakuwa na taarifa za kina kwa
kuwa hakuwa eneo la tukio.
Hata alipoulizwa jina la kitaalamu la bomu hilo alisema hana taarifa za kina.
Wakati Polisi wakieleza hayo, mashuhuda pamoja na taarifa zilizosambazwa
kwenye mitandao ya kijamii zilidai kwamba mtu mmoja alijeruhiwa kwenye
tukio hilo.
Taarifa zinaeleza kwamba mlipuko huo ulitokea baada ya Mnyika kwenda
kwenye gari ya Polisi kwa nia ya kuwasalimia na ndipo kishindo
kilichoashiria mlipuko wa bomu kilisikika.
Kufuatia tukio hilo, mkutano huo ulipigwa marufuku na kuhamishiwa eneo la Ubungo Mataa ambako ulifanyika.
Diwani wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob, akifungua mkutano huo
alisema waliamua kuchukua vibali viwili vya mkutano huo kwa tahadhari
cha Mabibo na cha Ubungo.
Akizungumzia kuhusu tukio hilo wakati akihutubia mkutano wa hadhara
uliofanyika Ubungo jana, Mnyika alidai kuwa waliomba kibali cha kufanya
mkutano huo siku tano kabla kwa kuwaandikia polisi barua, lakini
hawakuwajibu hadi jana asubuhi wakiwataka kusitisha kwa sababu kulikuwa
na ziara ya Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, kukagua shughuli
za usafi jijini Dar es Salaam.
Mnyika alisema aliwajibu polisi kuwa hawezi kupokea taarifa za kusitisha
mkutano wake huyo kwa simu bali aliwataka wampe kwa maandishi.
Alisema baadaye polisi waliandika barua ya kumuagiza asitishe mkutano wake huo kupisha ziara ya Makamu wa Rais.
Alisema hata hivyo, alipoangalia ratiba ya ziara ya Makamu wa Rais,
aligundua kuwa haikugusa jimboni mwake na kuwaomba tena polisi wamruhusu
kufanya mkutano huo.
Alisema alimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam,
Suleiman Kova na kujibiwa yuko nje ya nchi, hivyo aliwaomba wasaidizi
wake wampe kibali lakini hawamkujibu na kumuomba asubiri wajadiliane
kwanza.
Mnyika alisema kutokana na muda kuyoyoma, alimtafuta Mkuu wa Jesh la
Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema, kumuomba amsaidie, lakini
aligonga mwamba baada ya kumjibu kuwa hawezi kutengua maamuzi
yaliyotolewa na kiongozi wake wa chini na kumtaka aandike barua nyingine
ya kuomba kibali cha kufanya mkutano.
"Wakati naendelea kuwasiliana na viongozi wa polisi kuomba wanipe
kibali, nilikuwa tayari kwenye viwanja vya Sahara na ndipo zikaja
defender (magari ya polisi) tatu za polisi," alisema na kuongeza kuwa:
"Ziliposimama niliwafuata na kwenda kuwaambia kuwa vipi tena mbona
mmekuja wakati nimeomba kibali cha kufanya mkutano, ndipo lilipolipuka
bomu hilo ndani ya gari ambalo nami nilikuwa nimesimama karibu nalo."
Alisema baada ya kulipuka bomu hilo, watu walikuwa wamekusanyika katika
viwanja hivyo walikumbwa na taharuki na kukimbia ovyo kunusuru ya maisha
yao. Kwa mujibu wa Mnyika, wakati watu hao wakikimbia ovyo, alikwenda
lilikoangukia bomu hilo kumuwahi majeruhi, Thomas Jarome.
Alisema polisi nao walikwenda kumuwahi majeruhi huyo na kumbeba
'mzobemzobe' wakati wakitaka kumuingiza kwenda gari lao, Mnyika na
viongozi wengine wa Chadema waliwazuia na kumpeleka hospitalini ambako
alipatiwa matibabu na kuruhusiwa kuondoka.
Alisema wakati majeruhi huyo akiendelea kupatiwa matibabu, viongozi wa
chama hicho walikusanyika na kujadili sehemu nyingine ya kwenda kufanyia
mkutano wao na kubaini kuwa Diwani wao wa Ubungo alikuwa na kibali cha
kufanya mkutano eneo la Abiani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aliwatangazia wananchi wafuasi na wapenzi wa Chadema wakiwaomba wahamie Abiani.
Katibu wa Mbunge wa Ubungo, Gastone Garubindi, alidai bomu hilo
lilipigwa na polisi kwa lengo la kuwatisha wananchi wasihudhurie mkutano
huo.
Akizungumza na NIPASHE majeruhi Jerome, alidai kuwa polisi walikusudia
kulipua bomu hilo kwani lilikuwa mikononi mwao na askari waliopata
mafunzo ya kutosha kuhusu milipuko.
Alisema baada ya kujeruhiwa, viongozi wa Chadema walimpeleka katika
kituo Mabibo ambako alipewa PF3 na kwenda zahanati Tandale na kutibiwa.
Jerome alisema baada ya kutibiwa aliruhusiwa kurejea nyumbani na
kutakiwa kurudi leo kwa uchunguzi zaidi na kuchomwa sindano ya pepopunda
(tetanus).
Tukio la jana limekuja huku uchunguzi wa mlipuko wa bomu uliotokea Juni
15, mwaka huu katika viwanja vya Soweto, Kata ya Kaloleni mkoani Arusha
kwenye mkutano wa kufunga kampeni za udiwani wa Chadema, ukiwa bado
unaendelea. Katika tukio hilo, watu watatu walipoteza maisha na wengine
kadhaa kujeruhiwa vibaya. Bomu hilo linaelezwa kuwa lilipuka kwenye
mkusanyiko wa watu mita chache kutoka jukwa kuu, wakati mkutano huo
ulipokuwa umekwisha na shughuli ya kukusanya michango ikiendelea.
Viongozi wa juu wa Chadema, Freeman Mbowe na Godbless Lema walikuwapo kwenye eneo hilo.
Hadi sasa hakuna mtu ambaye amekamatwa kuhusiana na mlipuko huo pamoja
na kwamba Serikali imetangaza donge nono la Sh. milioni 100 kwa mtu
atakayefanikisha kukamatwa kwa mhusika au wahusika wa tukio hilo.
Zaidi ya watu 70 walijeruhiwa baada ya tukio hilo kufuatia polisi
kufyatua risasi za moto kwa nia ya kukabiliana na wananchi waliokuwa
wanawashambulia.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alikaririwa akieleza kwamba bomu lililolipuka Arusha lilitengenezwa China.
Aidha, Septemba, 2012 aliyekuwa Mwakilishi wa Kituo cha Chanel Ten
mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, aliuawa kwa kupigwa bomu la machozi na
askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) eneo la Nyololo Wilaya ya
Mufindi mkoani Iringa.
Alipigwa bomu hilo baada ya kupokea kipigo kutoka kwa baadhi ya askari
wa FFU waliokuwa wakiizuia Chadema kuendesha harakati zake za kufungua
tawi la chama hicho katika eneo hilo.
Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari
Mkoa wa Iringa (IPC), aliuawa mbele ya wananchi, askari wa FFU na
aliyekuwa Kamanda wa jeshi hilo mkoani humo, Michael Kamuhanda.
Askari huyo anayedaiwa kumuua Mwangosi, Pacificus Cleophase Simon (23),
alikamatwa na kufikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma za mauaji hayo
na kesi hiyo bado inaendelea kutajwa
0 comments: