Vita vya Ufaransa na Magaidi Mali
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian, ameelezea kile anachosema ni vita vya kweli vinavyoendelea nchini Mali baada ya makabiliano mapya kutokea karibu na mji muhimu Kaskazini mwa nchi.
Alisema kuwa wanajeshi wa Ufaransa wamepigana kile walichotaja kuwa wafuasi wa makundi hayo ya wapiganaji wanaopigana viungani mwa mji wa Gao
Mwandishi wa BBC mjini humo anasema kuwa aliweza kusikia sauti za milipuko.
Mji wa Gao ulikuwa ngome ya wapiganaji hao lakini maafisa wa Ufaransa walitangaza kuwa majeshi yaliweza kukomboa mji huo.
Wakati huohuo,mamia ya wapiganaji wa kiisilamu wameuawa nchini Mali tangu majeshi ya Ufaransa kuanza kupambana nao mwei jana.
Kwa mujibu wa waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian, wengi waliuawa katika mashambulizi ya angani pamoja na makabiliano ya moja kwa moja na wanajeshi wa Ufaransa.
Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje Laurent Fabius, amesema kuwa Ufaransa huenda ikaanza kuondoa wanajeshi wake Mali kuanzia mapema mwezi Machi.
Kwenye mahojiano kupitia kwa vyombo vya habari,alisema kuwa ikiwa kila kitu kitakwenda sawa, idadi ya majeshi huenda ikapungua.
Ufaransa ina takriban wanajeshi 4,000 nchini Mali. Hapo jana mkutano wa maafisa kutoka UN, EU na Afrika ulianza mjini Brussels kujadili hatua zitakazochukuliwa baada ya wanjeshi wa Ufaransa kumaliza kazi yao.
Aidha waziri wa ulinzi alisema kuwa mji uliokuwa umesalia kuwa chini ya waasi ,Kidal, tayari umedhibitiwa na majeshi ya Ufaransa.
Mashambulizi ya angani dhidi ya waasi yanaendelea katika maficho yao kaskazini mwa nchi.
Bwana Le Drien alisema kuwa wapiganaji hao walifariki katika mashambulizi ya angani, wengine waliuawa wakiwa kwenye magari yao, na wengine katika mashambulizi ya ardhini mjini Konna mwanzoni mwa kampeini ya kupambana na nao.
0 comments: