Chadema yawataja 10 utekaji Kibanda

Waenda mahakamani leo kuomba simu zao hadharani.

                Wamo wana usalama, waandishi wa habari na wanasiasa.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibua mapya katika sakata la kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, kwa kuwataja watu 10 waliodai kuwa ni wahusika wa matukio ya ugaidi nchini.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu njama za kuichafua Chadema zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyombo vya dola ukiwamo Usalama wa Taifa.

Marando ambaye alisema kuwa amepata taarifa hizo kutokana na ujuzi wake kama mwansheria na mtu ambaye amepata ujuzi wa kazi za ushushu, hivyo alifanya uchunguzi wa matukio hayo ya utekaji na utesaji na kugundua mambo mengi.

Waliotajwa kuhusika na matukio hayo ni pamoja na Waziri mmoja, maofisa wa Usalama wa Taifa watatu, akiwamo mmoja wa mwenye wadhifa wa juu, kada mwandamizi wa CCM, Mhariri Mtendaji mmoja wa gazeti, washitakiwa wawili wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi mahakamani, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na Ludovick Rwezahula.

Wengine ni ofisa aliyepata kufanya kazi Makao Makuu ya Chadema, Mwandishi na Mpigapicha mmoja wa magazeti ya serikali, mtoto wa kigogo serikalini na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Stephen Ulimboka.

Marando alisema leo, ataongoza timu ya mawakili wa Chadema kwenda mahakamani kuomba maelezo ya simu zao kutaka kampuni za simu za mikononi kuwasilisha maelezo ya mawasiliano yanayodaiwa kupanga njama za ugaidi na hususani utengenezaji wa video iliyomtia matatani Lwakatare.

Kutokana na sababu mbalimbali za kitaaluma na maadili, tumeamua kusitiri majina hayo kwa sasa, licha ya kutamkwa hadharani na Marando, huku tukiendelea kukamilisha wajibu wetu wa kiuandishi kabla ya kuwataja.

Marando ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema, alisema watu hao ni muhimu sana katika upangaji wa mkakati wa utengenezaji wa video ya Lwakatare na vitendo vya kihalifu vya utekwaji wa Kibanda na tukio la kutekwa na kisha kutupwa msituni kwa Dk.  Ulimboka.



Alisema Chadema inazo taarifa kuwa miongoni mwa watuhumiwa hao, kada mwandamizi wa CCM kwa sasa anafanya mipango na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni  ya simu ya Vodacom ili kumsaidia kufuta taarifa zake za mawasiliano aliyokuwa anayafanya na baadhi ya wanachama wa Chadema na maafisa usalama wa Taifa kufanikisha mkakati huo, kitu ambacho ni kinyume cha Sheria za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Alisema kada huyo na wenzake ndio waliopanga njama za utekaji wa Kibanda na wakatimiza lengo hilo.

Alisema CCM inatambua kuwa katika hali ya sasa hakiwezi kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ndiyo maana wanapanga kila mbinu chafu kuiangamiza Chadema.

Marando alisema kada huyo na wenzake walipanga kumteka Kibanda wakatimiza lengo hilo, baadaye wakaingia kwenye ‘Plan B’ ya kutaka kuihusisha Chadema kwa kumtumia Rwezahula ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi ya Lwakatare kufanikisha mkakati huo wa kishetani.

Alisema mwandishi na mpigapicha ni mtu muhimu sana mahakamani kwa kuwa ndiye aliyeandika ujumbe kwa njia ya barua pepe (email) kuipongeza ofisi binafsi ya Rais na Usalama wa Taifa kwa kupata video ya Lwakatare.

“Pongezi za (anamtaja mwandishi na mpiga picha huyo) kwa TISS (Idara ya Usalama wa Taifa) ndizo zinanisukuma kuiomba mahakama kuagiza kupatikana taarifa zake (anamtaja tena) anaipongeza TISS kwa kuibua njama za wahalifu, lakini mimi ninajua TISS ikipata njama za aina hiyo haraka inapeleka ushahidi polisi, lakini huu wa Lwakatare ulipelekwa YouTube badala ya kwenye vyombo vya sheria,” alisema Marando.

Alisema miongoni mwa mawasiliano hayo ni yale ya Disemba 28  mwaka jana siku ambayo mkanda wa Lwakatare umerekodiwa, Machi 4 na 6 mwaka huu ambayo ilikuwa ni siku moja kabla ya Kibanda kutekwa na yale ya usiku wa manane wa Machi 13 mwaka huu ambako mchana uliofuata Lwakatare kukamatwa.

“Mawasiliano na (anamtaja kada mwandamzi wa CCM) na (anamtaja ofisa wa Usalama wa Taifa) katika kipindi hicho nayo tunayahitaji kwa sababu huyu (anataja jina la Ofisa Usalama wa Taifa) anayetumia simu 0754 006355 mbali na kuwasiliana na (anamtaja kada mwandamzi wa CCM) ndiye aliyekuwa anawasiliana na mmoja wa waliomteka Dk. Ulimboka na ndiye aliyewasialiana na (anamtaka ofisa wa zamani wa Chadema) kati ya Januari 20 na Machi 6 mwaka huu,” alisema Marando.

Marando anamtaja Ofisa Usalama wa Taifa huyo kwa jina, kuwa anafanya kazi makao makuu na ndiye anayetumika kuendesha michezo ya kuhonga wanasiasa wa CCM na upinzani, na pia anapangia wabunge mambo ya kuongea kwa maslahi ya CCM.

Marando alimtaja ofisa usalama mwingine jina tunahifadhi kuwa ndiye aliyekutana na ofisa usalama wa Chadema, (jina tunahifadhi) na wenzake Machi 29 mwaka huu katika hoteli ya Sea Clif jijini Dar es Salaam.

Alisema katika mkutano huo, Ofisa Usalama huyo alimtaka Ofisa wa Chadema akubali kutumika kwa kutoa taarifa za vikao vya chama, kuwasilisha kwake nyaraka za Kamati Kuu na kueleza mipango ya Chadema katika kesi ya Lwakatare.

“Kwenye mpango huu, afisa huyo wa Usalama wa Taifa ambaye ninamfahamu vizuri alimuahidi … (anamtaja Ofisa wa Chadema) kiasi cha Sh. milioni 30 na kwamba fedha hizo angelipwa wiki iliyopita, aliahidiwa kwamba kila nyaraka atakayopeleka atalipwa ujira na kila mwezi atakuwa analipwa Sh. 500,000,” alisema Marando.

Ofisa Usalama wa Taifa huyo alipopigiwa simu na NIPASHE alimuuliza mwandishi kama hao Chadema wamemtaja kwa jina gani na baada ya kueleza alisema jambo hilo kwake ni jipya na kwamba ndiyo kwanza analisikia.

Ofisa Usalama mwingine anayetuhumiwa alipopigiwa simu na mwandishi kujitambulisha na kumweleza madai ya Chadema alikata simu wakati simu ya Ofisa Mwandamizi wa Usalama wa Taifa, simu yake ilikuwa haipatikani.

Kada mwandamizi wa CCM ambaye amekuwa akitajwa sana katika siku za hivi karibuni, simu yake ya kwanza ilipokelewa na mtu mmoja aliyedai siyo yeye na simu ya pili ilikuwa ikiita bila kupokewa.

Waziri anayetuhumiwa simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa, wakati mtoto wa kigogo mmoja serikalini alipotafutwa simu zake mbili zilikuwa hazipatikani; naye aliyepata kuwa mtumishi wa Chadema Makao Makuu, alipopigiwa simu ilipokewa, lakini baada ya mwandishi kujitambulisha aliikata.

Aidha, Mhariri anayetuhumiwa simu yake iliita bila kupokewa.

Hayo yameibuka wakati wananchi wakisubiri ahadi ya polisi kwamba ukweli juu ya nani hasa anayetuhumiwa kuhusika na sakata la kutekwa na kuteswa kwa Kibanda, angejulikana leo.

Wiki iliyopita, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issa Mngulu, alisema kuwa ripoti ya upelelezi wa timu maalum ya wapelelezi itatolewa kati ya Aprili 15, 16 au 17, mwaka huu.

0 comments:

Copyright © 2012 KARINGA NEWS Tz