CHAMA CHA TIBA ZA ASILI(ATME) WABARIKI MATUMIZI YA MAFUTA YA UBUYU, WASEMA HAYANA MADHARA YOYOTE KWA AFYA YA BINADAMU...!!


 

 

 

 

 

 

 

                                                                                                                                                                                                                        

Sasa ni kati ya Chama cha Tiba Asili (ATME) na  TDFA.  ATME kinadai hayana madhara wagonjwa wake wameyatumia kwa zaidi ya miaka 20.

Dar es Salaam. Mratibu wa Chama cha Watabibu wa Dawa za Asili Tanzania (ATME), Boniventure Mwalongo amesema taarifa zilizotolewa hivi karibuni na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TDFA) kuhusu matumizi ya mafuta ya ubuyu zinaweza kuleta madhara kwa jamii kwa sababu watu wengi wamekuwa wakiyatumia.

Akitolea mfano watumiaji wakubwa  wa mafuta hayo, Mwalongo alisema, wenye magonjwa kama ya moyo na wanaoishi na Virusi vya Ukimwi wamekuwa wakiyatumia mafuta hayo kwa muda mrefu na kudai yamewasaidia.

Mwalongo ameyasema hayo jana baada ya hivi karibuni kuibuka utata kuhusu ubora na usalama wa mafuta hayo na kudai kuwa wao kama ATME walianza kuyatumia kama dawa kwa wateja wao siku nyingi na hawajawahi kupata malalamiko yoyote na kuwahakikishia watumiaji kuwa hayana madhara.

 “Yametumika kwa zaidi ya miaka 20 na sisi tunazo kumbukumbu za wagonjwa tuliowapa mafuta hayo kama dawa na hatujawahi kupata ripoti yoyote ya madhara kwa wale waliotumia,” alisema Mwalongo.   TFDA ilitoa taarifa kwamba mafuta hayo hayafai kwa matumizi ya binadamu kwa sababu yana kiwango kikubwa cha tindikali ya mafuta aina ya cyclopropenoic fatty acids.

  Katika taarifa ya TFDA iliyotolewa juma lililopita ilisema athari zinazoweza kutokea kutokana na matumizi ya mafuta hayo ni pamoja na kuathiri vimeng’enyo vinavyosaidia katika uchakataji wa tindikali za mafuta mwilini.

  Pia ilisema ili yaweze kukidhi vigezo vya ubora na usalama ni lazima yafanyiwe usafishaji wakati wa usindikaji na kwamba kwa sasa nchini hakuna aina ya usindikaji unaofanyika wenye uwezo wa kuondoa tindikali hiyo ya cyclopropenoic fatty acids katika mafuta ya mbegu za ubuyu.

 Hata hivyo Mwalongo alikemea usambazaji holela wa mafuta hayo hasa baada ya kubainika kuwa yanatibu maradhi mbalimbali ambapo baadhi ya wajasiriamali wamekuwa wakiyasambaza wakati siyo wataalamu wa tiba asili.

  Mratibu huyo alizishauri mamlaka zinazohusika na suala zima la afya ya binadamu nchini kutoa majibu yatakayosaidia kuondoa mgawanyiko uliopo sasa kutokana na mafuta hayo badala ya kutoa taarifa za kutisha.

   Hata hivyo alipoulizwa Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Tiba Asili kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Paul Mhame, alisema hawana taarifa zozote kama kuna tafiti zimefanyika kuhusiana na matumizi ya mafuta hayo

 

 

 

 

 

 




 

 

 

 

 

 


0 comments:

Copyright © 2012 KARINGA NEWS Tz - Blogger Theme by SoraTemplates