Tendwa hana ubavu wa kuifuta Chadema

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, hana mamlaka yoyote ya kukifuta chama hicho.

Mbowe amesema kwa kufanya hivyo ni sawa na kuwataka wananchi wadai haki zao nje ya utaratibu rasmi, jambo alilosema ni la hatari kwa ustawi wa taifa.

Aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya malori iliyopo katika eneo la Majengo mjini hapa na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa Manispaa ya Songea na mikoa jirani ya Lindi na Mtwara waliofika  kushuhudia uzinduzi wa Kanda ya Kusini ya chama hicho.

Mbowe alisema kuwa binadamu yeyote pale anapodai haki yake, hapaswi kuzuiwa katika mazingira tatanishi, hivyo wanachama wa Chadema wana haki ya msingi ya kujiwekea ulinzi wao (Red Brigade) kama wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walivyojiwekea ulinzi wao kupitia vikundi vya Green Guard na si vinginevyo.

Alisema kuwa suala la Red Brigade siyo geni na wala halijaanzishwa na Mbowe, bali limewekwa bayana kwenye Katiba ya Chadema tangu mwaka 2006 ambapo linasema chama kitajiwekea ulinzi wa mali na viongozi wao, hivyo kuifuta Chadema ni kutafuta machafuko ndani ya nchi.

Mbowe alimtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuona umuhimu wa kuweka miundombinu ya kuwa na amani kwa kusimamia kikamilifu haki kwa vyama vyote vya siasa vilivyopo hapa nchini badala ya kuwa na upendeleo kwa CCM ambacho kinaonekana kuwa na propaganda nyingi kandamizi za kisiasa.

Alisema kuanzia sasa, Chadema itahakikisha kuwa inakuwa na ulinzi mkali kwa kuweka vikundi vya Red Brigade ambavyo vitakuwapo katika ngazi za serikali za mitaa, vijiji, tarafa, wilaya, mkoa na taifa.

Alifafanua kuwa kazi za vikundi hivyo itakuwa ni kulinda usalama wa mali za chama pamoja na viongozi wao.

"Red Brigade ilikuwapo tangu awali isipokuwa kwa hivi sasa kilichofanyika ni kuiongezea uwezo ambao umevifanya vyombo vya dola vishtuke na kuanza kuipigia Chadema kelele ingawa majukumu yake ni yale yale na yanaelekeana na vikundi vya Green Guard vya CCM.

Hata hivyo, Mbowe alisema kuwa vikundi vya  Green Guard vya CCM vimekuwa vikifanya matukio mengi ya kihalifu, lakini Jeshi la Polisi limekuwa likiyafumbia macho.

Alisema anayo mifano ya matukio ya uhalifu ya vikundi vya Green Guard, hakuyataja na kueleza kuwa wahalifu walikamatwa, lakini wakatoroshwa katika mazingira yenye utata.

Kuhusu rasimu ya Katiba, Mbowe amewahimiza wananchi kuwa makini anapoijadili.

Hata hivyo, alisema CCM inataka kuweka taratibu inazozitaka wakati Tume ya Katiba iliandaa vizuri, hivyo Chadema nayo ina mpango wa kuwa na tume yake ya kuijadili rasimu hiyo kwa kuwaelimisha wananchi mambo halisi yanayopaswa kuwapo katika Katiba mpya.      chanzo:chadema blog.

0 comments:

Copyright © 2012 KARINGA NEWS Tz