WATOTO 22 WAFARIKI DUNIA HII NI BAADA YA KULA CHAKULA CHENYE SUMU SHULENI
Baadhi ya watoto hao wakipatiw huduma hospitalini jana. |
Takribani watoto 22 wamekufa na
wengine wengi wanaumwa baada ya kula chakula cha bure shuleni mchana
ambacho kulichanganyika na dozi kubwa ya dawa za kuua wadudu, maofisa
nchini India walisema jana.
Haikuweza kufahamika mara moja jinsi kemikali hizo zilivyoingia kwenye chakula hicho kwenye shule moja iliyoko mashariki mwa jimbo la Bihar, ingawa mmoja wa maofisa alisema inawezekana chakula hicho hakikuwa kimeoshwa vema kabla ya kupikwa.
Watoto hao, wenye umri wa kati ya miaka 8 na 11, walianza kuumwa juzi muda mfupi baada ya kula chakula cha mchana shuleni kwao huko Masrakh, kijiji kilichopo maili 50 kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo hilo wa Patna.
Mamlaka za shule hiyo haraka zikasitisha kugawa chakula hicho cha wali, soya, dengu na viazi kufuatia watoto hao kuanza kutapika.
Chakula hicho cha mchana, sehemu ya kampeni maarufu ya nchi nzima kuwapatia chakula japo mlo mmoja watoto kutoka familia masikini, kilikuwa kimepikwa kwenye jiko la shule hiyo.
Watoto hao haraka walikimbizwa kwenye hospitali moja mjini humo na baadaye wakapelekwa Patna kwa matibabu, alisema msemaji wa serikali Abhijit Sinha.
Mbali na watoto hao 20 waliokufa, wengine 27 akiwamo mpishi wa shule walipelekwa hospitali, alisema. Kumi kati yao walikuwa katika hali mbaya.
Mamlaka zimemsimamisha kazi ofisa anayeshughulikia mpango wa mlo wa bure kwenye shule na kufungua kesi ya uzembe dhidi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo, ambaye alitoroka mara baada ya wanafunzi hao kuanza kuumwa.
P.K. Sahi, waziri wa elimu wa jimbo hilo, alisema uchunguzi wa awali umeonesha chakula hicho kilikuwa na kemikali ya organophosphate inayotumika kuulia wadudu kwenye mazao ya mpunga na ngano.
Inaaminika nafaka hiyo haikuwa imeoshwa kabla ya kupelekwa shuleni hapo, alisema.
Hatahivyo, wanakijiji walisema tatizo linaonekana kuwa upande wa chakula cha soya na viazi, wakaongeza kwamba watoto ambao hawakula chakula hicho walisalimika - ingawa walikula wali na dengu.
Mpango wa chakula cha mchana nchini India ni moja ya mipango mikubwa duniani ya lishe mashuleni.
Serikali za majimbo zina uhuru wa kuamua aina ya chakula na mida ya mlo huo kutegemea hali ya eneo husika na upatikanaji wa chakula hicho.
Kwa mara ya kwanza ilianzishwa kusini mwa India, ambako kulionekana kuwapo wazazi wengi mafukara wasio na uwezo wa kuwapeleka watoto wao shule.
Tangu hapo mpango huo umekuwa ukisambaa nchi nzima na kuwasikia zaidi wa watoto wa shule milioni 120 kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na utapiamlo.
Kwa mujibu wa serikali hiyo, karibu nusu ya watoto nchini India wanasumbuliwa na utapiamlo.
Ofisa wa ngazi ya juu aliyechaguliwa wa Bihar, Waziri Mkuu Nitish Kumar, ameamuru uchunguzi ufanyike kuhusu vifo hivyo.
Chanzo zero99
0 comments: