UPDATE:TAARIFA KAMILI KUHUSU BOMU KATIKA KANISA LA KKKT DAR ES SALAAM


POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imebaini kuwa chombo kilichodhaniwa kuwa bomu katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama hakikuwa bomu, bali ni kifaa cha Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) cha kuchunguza anga.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleman Kova alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari, baada ya kufanya uchunguzi kwa kushirikiana TMA.
"Baada ya kupata taarifa, polisi walifika eneo la tukio na kukuta kifaa kilicho katika umbo la kasha kikining'inia kwenye transfoma karibu na Kanisa kikiwa kinawaka taa.
“Katika kasha hilo kulikuwa na maandishi ya kalamu ya wino yaliyosomeka TMA na Airport," alisema Kamanda Kova.
Alisema baada ya uchunguzi wa awali, polisi walibaini kuwa kifaa hicho si bomu na kuondoka nacho kwa uchunguzi zaidi. Mtabiri Mwandimizi wa hali ya hewa kutoka TMA, Augustino Kanemba, alisema kifaa hicho kinaitwa Radio Sound na hutumiwa na Mamlaka hiyo kufanya utafiti wa hali ya anga za juu.
"Kifaa hiki hurushwa juu kuleta taarifa ya hali ya anga, kwa kawaida hufungwa puto ili kipae angani na baada ya kufika juu, puto hupasuka na kutua sehemu yoyote ya Dar es Salaam … hili si bomu," alisisitiza Kanemba.
Hata hivyo, Kamanda Kova alipongeza washarika wa Kanisa hilo, kwa kutoa taarifa Polisi na kuomba waendelee kufanya hivyo wanapoona kitu wasichokielewa.
Akizungumzia mlipuko katika Kanisa la KKKT, Usharika wa Segerea, Kamanda Kova alisema Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, kwa kushirikiana na wataalamu wa fani za ugaidi na matumizi ya mabomu kutoka makao makuu ya Jeshi hilo, wanafanya upelelezi kubaini waliohusika na tukio hilo.
Katika tukio hilo la Agosti 24 mwaka huu saa 8 usiku, waumini wapatao 20 wakiwa wanaendelea na ibada, ghafla walitokea watu wanne na kuingia kanisani na kutupa chupa ya bia ikiwa na utambi na mafuta yadhaniwayo kuwa ya taa eneo la madhabau na kusababisha mlipuko.
Katika hatua nyingine, Polisi imekamata wahalifu 180 wakiwamo majambazi katika msako ulioendeshwa na Jeshi hilo ndani ya wiki moja. Pia imekamata bastola mbili, risasi tisa, magunia mawili ya bangi na magari mawili ya wizi.



0 comments:

Copyright © 2012 KARINGA NEWS Tz