CHEKI WATOTO WACHANGA WANAVYOTUPWA! DU!!! INASIKITISHA SANA
Watoto wachanga baada ya kuzaliwa katika Manispaa ya Morogoro,
ongezeko la wazazi kutupa watoto wao limekuwa likiongezeka nchini. Picha
ya Maktaba.
Tarime. Waswahili husema, mapenzi matamu pale yanapokolea, lakini hugeuka shubiri pale yanapochacha.
Wengine huwanyonga, kuwatupa vichanga au watoto wadogo kwa sababu ya
kuchuja mapenzi au kwa sababu wamekubaliana na wenza wao wawaue watoto
labda kwa sababu hawafanani na mume.
Ukosefu wa uaminifu kwa wapendanao, hususan waliomo kwenye ndoa imekuwa
ni sababu ya wahusika kukata tamaa, jambo ambalo limesababisha watoto
wanaozaliwa kufanyiwa ukatili na hata kuuawa.
Utafiti uliofanywa katika wilaya hiyo umebaini kuwa watoto wengi
wanaozaliwa na kutupwa ni wale ambao wazazi wao ama wapo kwenye ndoa au
uchumba, ambao watu wake hawaelewani.
Kwa upande wa wanawake, yule aliyekuwa na uhusiano na mwanamume mwingine
na kwa bahati mbaya akapata ujauzito nje ya ndoa hujikuta akilazimika
kutoa mimba au kutupa mtoto pindi anapojifungua ili kunusuru ndoa au
uchumba.
Kadhalika, mwanamume anapomuhisi mkewe kuwa alikuwa na uhusiano ya
kimapenzi na mwanamume mwingine, ajifunguapo mtoto, humshawishi mke au
au yeye huwadhuru wote kwa pamoja.
Pia, mama akishajifungua na baba akaona mtoto hafanani naye, humshawishi
mama kumuua mtoto. Matendo haya jambo yanaonekana kupigiwa kelele mno
na vyombo vya dola, bado yanaendelea kwa siri kubwa katika baadhi ya
maeneo.
Ushuhuda na hali halisi
Ipo mifano kadhaa ya matukio kama hayo kwani wilayani Musoma mwaka 2011,
aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Robert Boazi ambaye kwa
sasa yuko Kilimanjaro aliwahi kuwakamata wazazi ambao walishirikiana
kuua mtoto na kisha kumtupa.
Kisa ni nini ?
Ni baada ya baba kudai kuwa mtoto yule aliyezaliwa si wake, bali mwanamke alipewa uja uzito na mwanamume mwingine.
Sufiani Mageta, ambaye ni Katibu wa Afya katika Hospitali ya Wilaya ya
Tarime anasema kuwa wao hupokea watoto wachanga wanaotupwa baada ya
kuzaliwa, baadhi yao hukutwa wakiwa hai na wengine wakiwa tayari
wamekufa.
Anasema kwa mwaka jana pekee, watoto watatu hai waliokotwa wakiwa
wametupwa na sasa wanalelewa katika kituo cha kulelea watoto yatima
kilichopo mjini Musoma.
Askofu Isaac Kitongo wa Kanisa la Jeshi la Wokovu, Divisheni ya Tarime
anasema kuzaa mtoto nje ya ndoa husababisha baadhi yao kutelekezwa.
Ofisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Magreth Segu anasema:
”Wanaume wa siku hizi wengi, wao wanakataa kuishi na mtoto wa kambo,
hata wakiishi nao wanawanyanyapaa na wengine wamefikia hatua ya kuwaua
kwani anaona ni aibu kwa rafiki zake kuwa ameoa mwanamke mwenye mtoto”.
Abel Gicheina, Ofisa wa Ustawi wa Jamii katika Hospitali ya Wilaya ya
Tarime anasema: “Siku hizi wengi wanaonekana wanaingia kwenye uhusiano
kwa kuwa na tamaa zaidi ya upendo wa kweli”.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Tarime, Mwasiti Itumbo anasema kuwa
zaidi ya kesi 20 zimeripotiwa mwaka jana ofisini kwake na zote
zinazohusu wanandoa kutoka nje ya ndoa na tatizo la wanaume kutokutoa
huduma ya matunzo kwa watoto wanaowazaa.
Itumbo anasema kuwa wanaume hudai kuwa hawatoi matunzo kwa watoto wanaozaliwa kwani wanakuwa si damu yao.
Wanawake kwa upande wao, wanajitetea kuwa wanatoka nje ya ndoa kutokana
na baadhi ya wanaume kutotoa matumizi ya kutosha kwa familia zao, badala
yake wengi wao huwajali zaidi wanawake wa nje ya ndoa.
Ingawa si wote wenye tabia hii ya kutoka nje ya ndoa, jambo hilo, ofisa
huyo anasema ndilo linalowafanya wanawake nao watoke nje ya ndoa
kutafuta watu wa kuwapa mahitaji, baadhi yao hujikuta wamepachikwa uja
uzito nje ya ndoa.
Lucy John, mkazi wa Tarime (si jina lake halisi) anasema kuwa baadhi
ya wasichana ambao hawajaolewa wakiwamo wanafunzi wanasema kuwa
wataacha kutoa mimba iwapo wanaume wanaowabebesha mimba watakuwa tayari
kulea watoto kwani wengi wao wamekuwa wakikataa ujauzito na wanaposhtaki
polisi hawaoni hatua za kisheria zikichukuliwa dhidi ya wanaume.
Kauli ya RPC
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Justus Kamugisha
anasema kuwa kwa mwaka 2011-2012, zaidi ya watoto wanane wachanga
walikutwa wametupwa wamekufa na wengine wakiwa hai na kuongeza kuwa
watuhumiwa watano walifikishwa mahakamani.
Wengine wamehukumiwa kifungo na kesi nyingine zimefutwa kwa kukosekana
ushahidi na sababu mojawapo kubwa ni kutokana na jamii kutokusaidia
kutoa ushirikiano Polisi wakati wa upelelezi.
Kamanda Kamugisha anaitaka jamii kushirikiana na polisi kuwafichua
wale wanaobeba mimba na kisha kutoa mimba au kuua watoto wao ili
wachukuliwe hatua zi kisheria.
Anaeleza kuwa jamii ndiyo ipo karibu na wahusika wa tukio, wamekuwa
hawako wazi kuwafichua waovu, jambo ambalo linawapa ugumu polisi wakati
wa upelelezi wao, kiasi kwamba wengine huficha watuhumiwa.
Mwananchi
0 comments: