Rais Kikwete aongoza waombolezaji
Rais Jakaya Kikwete akimfaliji Mke wa
marehemu Dk Sengondo Mvungi, Anna Shayo, nyumbani kwa marehemu, eneo la
Kibamba jijini Dar es Salaam jana.PICHA|MICHAEL JAMSON
Dar es Salaam. Rais
Jakaya Kikwete ameeleza kushtushwa na kufadhaishwa na taarifa za kifo
cha Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi
kilichotokea juzi kwenye Hospitali ya Millpark, Johannesburg, Afrika
Kusini.
Mwili wa Dk Mvungi unatarajiwa kuletwa kesho na mazishi yake yamepangwa
kufanyika Jumatatu ijayo, Kisangara, Wilaya ya Mwanga Mkoa wa
Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi ambaye pia ni msemaji wa familia, James
Mbatia alisema mipango ya kuleta mwili wa Dk Mvungi ilikuwa inakwenda
vizuri ikiratibiwa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Radhia Msuya na
mwanaye Dk Mvungi, Deogratius Mwarabu.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana ilisema kuwa Rais Kikwete alimtumia
salamu za rambirambi, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba na
kueleza kuwa amepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Dk Mvungi.
“Kwa hakika ni taarifa iliyonisumbua na kunipa huzuni nyingi,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema kuwa hakuna shaka kuwa katika maisha yake, Dk
Mvungi ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa namna
mbalimbali na kuwa kifo kimemfika wakati Taifa la Tanzania lilikuwa bado
linahitaji busara, hekima na mchango wake katika mchakato mzima wa
kusaka Katiba Mpya.
Aongoza waombolezaji
Rais Kikwete jana aliongoza maelfu ya waombolezaji kutoa pole kwa
familia ya Dk Mvungi nyumbani kwake Kibamba-Msakuzi, Dar es Salaam.
Rais Kikwete ambaye alifuatana na mkewe, Salma alitia saini kitabu cha
maombolezo na kumpa pole mjane wa Dk Mvungi, Anna Shayo na ndugu na
jamaa wengine kabla ya kuzungumza faragha kwa muda na Jaji Warioba
ambaye alikuwapo msibani hapo pamoja na wajumbe karibu wote wa tume
yake.
Viongozi wengine waliokuwapo ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na Naibu wake, Angela Kariuki.
Pia kulikuwa na mamia ya waombolezaji wakiwamo wakazi wa maeneo ya jirani, wanasiasa, wasomi na viongozi wa Serikali.
Tume kusimamisha shughuli
Akizungumza msibani hapo jana, Jaji Warioba alisema shughuli za tume zitasimama hadi mazishi ya mjumbe huyo yatakapomalizika.
“Tumesitisha shughuli za tume hadi kipindi cha msiba kitakapomalizika.
Baada ya hapo tutaendelea kuandaa rasimu ya pili ya Katiba,” alisema
Jaji Warioba.
NCCR bendera nusu mlingoti
Chama cha NCCR-Mageuzi kimetangaza maombolezo ya siku saba kutokana na
kifo cha Dk Mvungi ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki
za Binadamu wa chama hicho.
Mbatia alisema katika maombolezo hayo, bendera za chama hicho zitapepea nusu mlingoti nchi nzima kuanzia jana.
Alisema kumekuwa na mshikamano mkubwa baina ya Serikali, Chuo Kikuu Dar
es Salaam, wanafamilia na chama chake na kumshukuru Rais Kikwete kwa
ushirikiano wake.
Mwananchi
0 comments: