Sumry yatoa ubani wa Sh 5.5M ajali Singida
Kholani alisema pia Mbunge wa Singida Magharibi,
Mohamed Missanga ametoa Sh600,000 na wakazi wa Tarafa ya Ihanja waishio
jijini Dar es Salaam pia wamechanga Sh600,000.
Uongozi wa Kampuni ya Mabasi ya Sumry ya Sumbawanga, Rukwa umetoa ubani wa Sh5.5 milioni kwa familia za ndugu na jamaa waliofariki dunia kutokana na ajali ya moja ya mabasi yake iliyotokea Aprili 28 katika Kijiji cha Utaho, Wilaya ya Ikungi, Singida.
Katika ajali hiyo, watu 19 wakiwamo polisi wanne,
walifariki papohapo baada ya kugongwa na basi hilo lililokuwa likitoka
Kigoma kwenda Dar es Salaam.
Ajali hiyo ilitokea baada ya ajali ya kwanza
iliyolihusisha lori na mwendesha baiskeli ambaye alipoteza maisha katika
eneo hilo baada ya kugongwa na lori hilo. Wakazi hao waliogongwa
walikuwa wamekusanyika kushuhudia ajali hiyo.
Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Hipoliti Daniel
Kholani alisema rambirambi hiyo ilikabidhiwa kwa Serikali ya Kijiji na
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone ambaye naye alichangia
Sh100,000.
Kholani alisema pia Mbunge wa Singida Magharibi,
Mohamed Missanga ametoa Sh600,000 na wakazi wa Tarafa ya Ihanja waishio
jijini Dar es Salaam pia wamechanga Sh600,000.
“Tangu kutokea kwa ajali hiyo kijiji kimeendelea
kupata idadi kubwa ya wageni kutoka sehemu mbalimbali kuja kutoa pole
kwa wafiwa. Tunatarajia kufanya sala maalumu kwenye eneo la tukio kesho
(leo), kuwaombea ndugu zetu.”
Kholani alisema wakazi wa kijiji hicho, Mussa
Mohammed, Suku Abdallah na Ayubu Ramadhani bado wamelazwa hospitalini
wakiendelea kutibiwa majeraha waliyoyapata kwenye ajali ya basi hilo
ambalo bado lipo Kituo cha Polisi Ikungi.
0 comments: