NAIBU MEYA AMPANDA KIZIMBANI
NAIBU Meya wa Jiji la Arusha, Prosper Msofe na Diwani wa Kata ya
Levelos, Ephata Nanyaro, wote kutoka CHADEMA, wamefikishwa mahakamani
kwa kosa la kumshambulia mgambo wa jiji, William Mollel.
Mwanasheria wa Serikali, Mary Lucas, aliwasomea shitaka hilo la
jinai namba 413/2014 jana mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya
Arumeru, Patricia Kisinda.
Alisema kuwa Aprili 16 mwaka huu, wakiwa maeneo ya Levelos, madiwani
hao wanadaiwa kumpiga, Mollel kifuani na sehemu mbalimbali za mwili,
hivyo kumsababishia maumivu mwilini.
Lucas alisema kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, hivyo
akaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo, huku
akiweka wazi kuwa upande wa serikali hauna pingamizi ya dhamana kwa
washitakiwa hao.
Madiwani hao walikana shitaka hilo na wako nje kwa dhamana hadi
upelelezi utakapokamilika ambapo shauri hilo litarudi mahakamani hapo
kwa ajili ya kutajwa Julai 8, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, wananchi kadhaa walionekana wakiwa na barua
kwa ajili ya kuwadhamini madiwani hao ambao juzi walitangaza kuwa
hawako tayari kudhaminiwa ili waende mahabusu kwenye gereza la Kisongo.
0 comments: