SAFARI ZA MIKOANI SASA UTATA...! MALORI NA MABASI FUL MGOMO... CHEKI HAPA
Siku moja baada ya Chama cha Wamiliki wa Malori nchini (TATOA), kutangaza usimamishaji huduma za kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi kuanzia leo, Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani (TABOA), nacho kimetangaza usitishaji huduma zake (kusafirisha abiria), kuanzia kesho
. Awali TATOA kilidai, lengo la kusitisha huduma ni kupinga agizo la Serikali kupitia Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli kuondoa msamaha wa tozo ya uzito wa magari yaliyozidi asilimia tano ya uzito unaokubalika kisheria.
Msemaji wa TATOA, Bw. Elias Lukumay, alisema msamaha huo ulitolewa na Serikali mwaka 2006 baada ya kamati ambayo iliundwa na Serikali ikishirikisha kufanya ziara katika mizani na kubaini haziko sawa kwa maana ya kutofautiana vipimo vyake.
Sababu nyingine iliyosababisha Serikali kutoa msamaha huo ni ubovu wa barabara, matuta mengi yaliyosababisha kuyumba kwa mzigo na mizani kutofanyiwa matengenezo.
Alisema uamuzi huo wa Serikali haukuishirikisha TATOA kama ilivyofanya mwaka 2006 mbali ya umuhimu wa sekta hiyo nchini hivyo ili kuepusha mgogoro na Serikali pamoja na wafanyakazi wa mizani, wamekubaliana kupaki magari yao.
Wakati TATOA ikitoa msimamo huo ambao utekelezaji wake unaanza leo, TABOA nao wamemtaka Dkt. Magufuli kurudisha msamaha wa asilimia tano vinginevyo wanasitisha huduma za kusafirissha abiria kwenda mikoa mbalimbali nchini pamoja na nje ya nchi kuanzia kesho.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TABOA, Enea Mrutu, alisema kitendo cha kuondoa asilimia tano kutayafanya mabasi mengi kusafiri na abiria wachache hivyo wamiliki wake kuingia hasara.
Alisema tangu kutolewa kwa taarifa hiyo, kumekuwa na misururu mikubwa ya magari katika mizani hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria na kumaliza safari zao muda mbaya.
"Tunamuomba Dkt. Magufuli arudishe msamaha wa asilimia tano aliouondoa, upo uwezekano mkubwa wa mabasi kusafiri na abiria wachache hivyo kuingia hasara," alisema.
Alimtaka Dkt. Magufuli na Waziri wa Uchukuzi Dkt. Harrison Mwakyembe, kutafakari uamuzi huo kwa kina ili kutoka na jawabu la kurudisha msamaha huo kwani sekta hiyo inategemewa na wananchi wengi wanaosafiri kila siku.
"Tumekuwa hatushirikishwi katika masuala kama haya, kitendo cha Serikali kuyaruhusu magari aina ya Noah yenye thamani ndogo kubeba abiria zaidi ya uwezo wake pia hatukushirikishwa," alisema.
Wakati huo huo, Bw. Mrutu aliwataka wamiliki wote wa mabasi kufika katika Ofisi za TABOA ili kuchukua fomu kwa ajili ya kupunguziwa bima kwa asilimia tano.
Aliwataka na wamiliki ambao hawajajiunga na TABOA,wafanye hivyo sasa ili waweze kushirikiana katika mambo muhimu yanayohusu huduma wanayoitoa kwa abiria
Majira
0 comments: