Chadema yasema Zitto aliponzwa na waraka tu
Mwanasheria
Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwaambia waandishi wa habari Dar es
Salaam jana kwamba waraka huo unaeleza mbinu za uasi ambazo zililenga
kufanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani
wa chama hicho jambo ambalo ni kinyume na katiba, sheria na itifaki za
Chadema.
Hivi
karibuni, Kamati Kuu ya Chadema iliwavua nyadhifa zao, Zitto, Mjumbe wa
Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson
Mwigamba kutokana na madai hayo.
Siku tatu
zilizopita, Zitto na Dk Kitila waliitisha mkutano wa wanahabari na
kueleza sababu mbalimbali za kung’olewa kwao ikiwamo suala la posho na
ruzuku za vyama vya siasa.
“Wamefukuzwa
katika uongozi kutokana na kuandaa mpango wa mapinduzi uliopo katika
waraka wa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013,” alisema Lissu na kuongeza:
“Hawa wote
hawakuvuliwa madaraka kwa sababu ya taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC), kuhusu ukaguzi wa hesabu za chama, suala la posho
kwa wabunge wala kuuza majimbo ya uchaguzi mwaka 2010.”
Alisema
kutokana na kosa hilo, Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chadema ilikutana
juzi kupitia uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu na kuridhika nao, “Leo
(jana) wahusika wote watapatiwa barua zao zilizoorodhesha makosa yao
kumi na moja wanayotakiwa kujibu ndani ya siku 14.” Bila ya kuyataja,
Lissu alisema makosa hayo yote yamejikita katika waraka huo.
Mnyika pia
alijibu hoja zilizotolewa na Wakili wa kujitegemea na Diwani wa Kata ya
Mabogini mkoani Kilimanjaro (Chadema), Albert Msando juu ya kasoro
wakati wa kutoa hukumu kwa makosa ya Zitto na Dk Kitila, ikiwa ni
pamoja na kukiukwa kwa katiba ya chama inayoeleza kuwa mtu hatachukuliwa
hatua za kinidhamu kabla ya kupewa mashtaka kwa maandishi na mamlaka
husika na kupewa nafasi ya kuyajibu kwa maandishi.
Mnyika
alisema, “Zitto na Dk Kitila hawakumwambia wakili wao ukweli kwamba
kanuni hii ya chama ilishafanyiwa marekebisho muda mrefu na Baraza Kuu
la chama na kuongezwa kifungu (d), ambacho kinasema: “Kamati Kuu inaweza
kuchukua hatua za dharura kama inaona masilahi ya chama yanaathiriwa.”
Waraka
Mnyika
alisema waraka uliowang’oa Zitto na Dk Kitila ambao umechapishwa katika
magazeti mbalimbali pamoja na mitandao ya kijamii, siyo ule
uliowasilishwa katika Kikao cha Kamati Kuu.
“Waraka
utakaotumika katika mashtaka yao siyo huo. Sisi tutautumia ule ambao
uliwasilishwa katika Kamati Kuu ambao una mambo makubwa na mengi zaidi
kuliko huo unaochapishwa sehemu mbalimbali, ikibidi tutautoa huo waraka
halisi,” alisema.
Naye Lissu
alisema kuwa kitendo cha kuandaa mkakati huo ni kinyume na utaratibu na
kanuni za chama hicho, kufafanua kuwa ndiyo maana Chadema mwaka jana
kilitengeneza mwongozo wa wanachama kutangaza kusudio la kuwania uongozi
ndani ya chama, mabaraza yake na Serikali.
Alisema ni makosa kupanga mkakati wa kutaka kumweka mtu madarakani bila kutangaza au kumwambia mtu yeyote.
Kuhusu PAC
Lissu alisema masuala ya PAC yalizungumzwa katika kikao cha Kamati Kuu, lakini hayakuwa miongoni mwa hoja za kumng’oa Zitto.
Alisisitiza
kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alishindwa
kuvikagua vyama vya siasa kwa sababu hakuwa na fedha za kufanya hivyo,
kwamba jambo hilo alilieleza wazi na vyama pamoja na Msajili wa Vyama
vya Siasa walilipinga.
“Leo hii,
mwaka mmoja baadaye Zitto anaibuka na badala ya kusema CAG ameshindwa
kukagua hesabu za vyama, anasema vyama vimekataa kukaguliwa.
Alisema kuna nyaraka ambazo Zitto akiwa Naibu Katibu Mkuu alitakiwa kuzifahamu.
Alisema
Oktoba 15 mwaka huu, siku ambayo Zitto aliibua tuhuma za vyama
kutokaguliwa, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
alimwandikia barua CAG akimweleza kuwa wajibu wa kukagua vyama vya siasa
ni wa kwake na hatakiwi kulipwa na vyama hivyo, wala Ofisi ya Msajili
wa Vyama.
Mnyika
alisema matukio yaliyotokea mkoani Kigoma baada ya Zitto kuvuliwa
uongozi, ikiwa ni pamoja na kuchomwa moto bendera za chama hicho na
kuharibiwa kwa baadhi ya majengo ni mchezo wa kuigiza na uhuni
uliofanywa na watu ambao si wanachama wa Chadema.
Ratiba ya Uchaguzi
Awali,
Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema hicho, Benson Kigaila
alieleza maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu kujipanga kuanzia
ngazi ya chini mpaka taifa.
Pia aligusia
suala la kugatua madaraka kutoka makao makuu kwenda katika Kanda 10
pamoja na Progamu ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), ambayo utekelezaji
wake ulikuwa na awamu nne unaombatana na mafunzo mbalimbali.
Kuhusu
uchaguzi, alisema kuanzia Novemba 22 hadi 14 Desemba, mwaka huu ni
kipindi cha kukamilisha usajili wanachama kuanzia ngazi ya chini.
“Tarehe 15
Desemba mpaka 15 Januari, 2014 utafanyika uchaguzi katika ngazi za
vitongoji. Kuanzia tarehe 16 Januari hadi 30 Januari, 2014 kitakuwa
kipindi cha kukata rufaa na kukagua ukamilifu wa uchaguzi wa ngazi
hiyo,” alisema Kigaila na kuongeza:
“Februari 1
hadi 15 mwaka 2014, utafanyika uchaguzi ngazi za matawi (vijiji kwa
vijijini na mitaa kwa mjini), kuanzia Februari 16 hadi 29, itakuwa
kipindi cha kukata rufaa na ukaguzi kwa ngazi hiyo.”
Alisema kuwa
kuanzia Aprili Mosi hadi 10, 2014 utafanyika uchaguzi ngazi ya majimbo
ya uchaguzi ambayo yapo 236 na kuanzia Aprili 25 mpaka Mei 5, 2014
utafanyika uchaguzi ngazi ya wilaya.
Alisema
kuanzia Mei 20 mpaka 25, 2014 utafanyika uchaguzi ngazi za mkoa na Juni 6
hadi 9, 2014 utafanyika uchaguzi katika Kanda zote 10 na Juni 23 mpaka
30, 2014 utafanyika uchaguzi ngazi ya taifa.
0 comments: