'BABU SEYA, PAPII LAZIMA WATAACHIWA HURU'




NGUZA Mbangu, mtoto mkubwa wa mwanamuziki mahiri wa muziki wa dansi anayetumikia kifungo cha maisha jela, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya, amesema mzazi wake pamoja na mdogo wake, Papii, ni lazima wataachiwa huru hivi karibuni.

Mbangu, ambaye pia hufahamika kisanii kama Mashine, ambaye hivi sasa ni mwinjilisti, alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipozungumza na gazeti hili, akisema kuwa kutolewa jela kwa ndugu zake hao, kutawafanya Watanzania kumsujudia Mungu kupitia tukio hilo.

“Amini nakuambia, Mungu amenipa maono, Babu Seya na Papii wako huru, watatoka tu, kinachosubiriwa ni muda tu ambao hauko mbali, ni lazima watatoka kwa sababu hawana hatia,” alisema Mbangu, ambaye pia alihukumiwa kifungo cha maisha jela kama mzazi wake, lakini akaachiwa wakati walipokata rufaa kwa mara ya kwanza mahakamani.

Alisema tukio hilo litakapotokea, litawafanya Watanzania wote kumsujudia mwenyezi Mungu, kwa sababu litakuwa ni ishara ya uwezo wake katika kutenda maajabu.

Babu Seya na Papii walihukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 2004 baada ya kupatikana na hatia ya kuwanajisi watoto wa Shule ya Msingi Mashujaa iliyopo Sinza. Hata hivyo, jitihada zao za kujinasua kwa mara ya mwisho ziligonga mwamba hivi karibuni baada ya jopo la majaji watatu kutupilia mbali maombi ya kuachiliwa huru baada ya kufanya mapitio ya kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi nchini.

0 comments:

Copyright © 2012 KARINGA NEWS Tz