Mvua zaleta balaa Arumeru,barabara ya Arusha-Dodoma hatarini kukatika
FAMILIA kadhaa katika kijiji cha Meseyeki,Kisongo wilayani Arumeru zimenusulika kusombwa na maji baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji yaliyojaa ndani kwa zaidi ya masaa 10, kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi na kusababisha uharibiru mkubwa wa mali.
.Aidha barabara ya Arusha -Dodoma katika eneo hilo,ipo hatarini kukatika muda wowote iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kutokana na sehemu kubwa kumegwa na maji yanayotiririka kutoka mto Kagera uliopob wilayani humo.Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo wamemtupia lawama mkandarasi anayejenga barabara ya Arusha Minjingu wa kampuni ya Sogea Satom ya nchini Ufaransa ,kwa kushindwa kuweka madaraja kwenye mkondo wa maji badala yake ameweka makaravati ya bati ambayo ni madogo yaliyoshindwa kuhimili wingi wa maji.
Mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo,Julita Daud alisema kuwa maisha yao yapo hatarini kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kuwa kubwa, kwani maji yanayotiririka kutoka mto huo,yameshindwa kupita kwenye karavati za barabarani na kuishia kwenye makazi ya wao,hivyo ameiomba serikali kupitia wakala wa barabara TANROADS kuingilia kati ili kunusulu maisha yao.
Alisema siku hiyo akiwa ndani yeye na familia yake majira ya saa 3.45 walishtukia maji yanaingia ndani mwao na alipotoka na kuchungulia nje alishangaa kuona baadhi ya kuta za nyumba yake zikiwa zimebomoka ,huku uharibifu huo akikadilia kufikia shilingi milioni 50.
''kwakweli vitu vyangu vingi vimeharibika hapa tulipo tupo hatarini ,tunaomba serikali itusaidie ,kwani tupo katika wakati mgumu siwezi kupata usingizi nikihofu kuvamiwa na maji''alisema
Mkazi mwingine,Billy Graham Mathew alisema kuwa maji hayo yamesababisha uharibifu mkubwa baada ya ukuta wa nyumba yake kusombwa na maji huku sehemu kubwa ya nyumba zake zikipatwa na nyufa.
Alisema hali hiyo inatokana na kuziba kwa karavati zilizowekwa na mkandarasi wa kampuni hiyo ,kuwa ndogo na kushindwa kuhimili kishindo cha wingi wa maji hayo yanayotoka kwenye mkondo wa mto kagera.Aliongeza kuwa hali hiyo imesababisha watoto wao kutokwenda shule na baadhi ya huduma muhimu kutopatikana.
Naye meneja wa TANROADS mkoani Arusha,Deosdedit Kakoko,alipoulizwa juu ya athari hizo alisema kuwa ,Tanroads imetuma maombi ya kuomba fedha serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa daraja kubwa kwa kuwa makaravati yaliyopo ni ya muda mrefu yanasitahili kubadilishwa.
Hata hivyo aliongeza kuwa wananchi wanaoishi maeneo hayo wamechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo na ujenzi wa makazi,hali iliyosababisha mikondo ya maji ya zamani kuvurugika na kumomonyoka kwa udongo unaoziba kwenye karavati hizo.
0 comments: